Jumatatu 2 Novemba 2026 - 00:15
Kauli za Sheikh wa Al-Azhar za Kutetea Madhehebu ya Jaafaria Zinaonesha Uhalali wa Fatwa za Wanazuoni wa Madhehebu Hayo

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi, Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf, katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa, akigusia mijadala mikubwa iliyoibuka katika vyombo vya habari kuhusu “Sheria ya Hali Binafsi kwa mujibu wa Madhehebu ya Jaafaria”, alisisitiza uhalali wa madhehebu hayo na kueleza kuwa msimamo huo unaafikiana na kauli za Sheikh wa Al-Azhar.

Kwa mujibu wa ripota wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi, Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf, katika hotuba za Swala ya Ijumaa alizozitoa katika Husainiya Kuu la Fatimiyya mjini Najaf Ashraf, alizungumzia masuala mbalimbali ya ndani, ya kikanda na ya kimataifa.

Kutetea madhehebu ya Jaafari na Sheria ya Hali Binafsi

Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf, kuhusu mijadala mikubwa iliyoibuka katika vyombo vya habari kuhusiana na Sheria ya Hali Binafsi kwa mujibu wa Madhehebu ya Jaafaria, ambayo ilipitishwa na Bunge la Iraq, alisema: “Mjadala huu mkubwa unaibuliwa wakati ambapo Sheikh wa Al-Azhar tayari alikuwa amebainisha wazi kwamba Madhehebu ya Jaafaria ni madhehebu ya tano, na kwamba sisi katika Darul-Iftaa, wakati mwingine, hurejea katika fatwa za madhehebu haya ili kutatua matatizo ya kifamilia na kuzuia kusambaratika kwa familia.” Aliongeza kuwa; kauli hizi zinaonesha usahihi na uhalisia wa fatwa za Madhehebu ya Ahlul-Bayt (as).

Ukiukwaji wa mamlaka ya Iraq na vitisho vya kiusalama

Katika sehemu ya hotuba yake iliyohusu masuala ya ndani, akieleza wasiwasi wake kuhusu hali ya usalama wa anga ya nchi hiyo, alisema: “Anga ya Iraq bado inaendelea kukiukwa mara kwa mara na ndege za utawala wa Kizayuni pamoja na ndege zao za kujaza mafuta. Matukio haya ya wazi ya safari za ndege hizo yanatufanya tudai kuchukuliwa msimamo rasmi na thabiti dhidi ya ukiukwaji huu wa mamlaka ya Iraq.”

Hatupaswi, kutokana na shinikizo la nje, kuyatoa mhanga maslahi ya Iraq kwa kuiwekea Iran vikwazo

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Qabanchi, kuhusu masuala ya kikanda, alisema: “Kuna shinikizo kutoka baadhi ya pande za nje zinazotaka tukatishe uhusiano wetu na Iran. Sisi tunaamini kwamba Iran itaendelea kuwepo; kwa hiyo, hatupaswi kuyatoa mhanga maslahi yetu kwa kukata uhusiano nayo au kuiwekea mzingiro. Hata hivyo, pia hatuna nia ya kukata uhusiano wetu na jumuiya ya kimataifa.”

Aidha, akigusia mkutano wa pande nne uliofanyika Tehran, alisisitiza kuwa; utatuzi wa matatizo ya eneo hili unaweza kupatikana tu kupitia nchi zenyewe za eneo hilo, na si kwa njia ya uingiliaji wa mataifa ya nje.

Uhusiano na Kuwait na kuiunga mkono Yemen

Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf, akizungumzia uhusiano na Kuwait, aliueleza kuwa ni uhusiano unaojengwa juu ya utambulisho wa pamoja, ujirani na maslahi ya pande zote. Vilevile, akikosoa baadhi ya hukumu zilizotolewa dhidi ya wanazuoni wa dini katika eneo hilo, alitaka maamuzi dhidi ya Madhehebu ya Jaafaria yapitiwe upya.

Katika sehemu ya hotuba yake iliyohusu masuala ya kimataifa, baada ya kupongeza ustahimilivu wa wananchi wa Yemen na vikosi vya Ansarullah mbele ya mashambulizi makubwa, aliongeza: “Licha ya mashambulizi 119 yaliyofanyika katika kipindi cha saa 24 zilizopita na ushiriki wa nchi mbalimbali, tunashuhudia maendeleo makubwa ya vikosi vya Ansarullah. Sasa tunapaswa kujiuliza: Ni nani anayenufaika na vita hivi? Ni maadui wa Uislamu pekee wanaonufaika.” Aidha, aliiomba Saudi Arabia kurejea katika njia ya mazungumzo na kujitenga na njia ya uhasama dhidi ya Uislamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha